Jumanne 10 Novemba 2026 - 00:00
Watafiti kutoka Iran, Iraq na Lebanon Washiriki Utangulizi wa Kongamano la Kuadhimisha Miaka 1,000 ya Hawza ya Najaf

Hawza/ Watafiti kutoka Iran, Iraq, Lebanon na vituo vingine vya kielimu wameshiriki katika kongamano la pili la kimataifa la maandalizi ya kuadhimisha miaka 1,000 tangu kuanzishwa Hawza ya Kidini ya Najaf Ashraf, ambapo walijadili urithi wa kielimu wa Hawza hiyo katika karne za tisa hadi kumi na mbili za Hijria.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, kongamano la pili la kimataifa la maandalizi ya kuadhimisha miaka 1,000 tangu kuanzishwa kwa Hawza ya Kidini ya Najaf Ashraf lilifanyika mjini Najaf Ashraf, tarehe 30 Mehr na 1 Aban 1405 Hijria Shamsia, kwa kushirikisha kundi la wanazuoni, walimu na watafiti kutoka Hawza za Najaf na Qum, pamoja na watafiti kutoka nchi mbalimbali.

Tukio hilo la kielimu lilikuwa mkutano wa pili wa maandalizi kuelekea kufanyika kwa kongamano kuu la kuadhimisha miaka 1,000 ya Hawza ya Kidini ya Najaf, ambalo linatarajiwa kufanyika katika siku za usoni.

Kongamano hilo la maandalizi lilikuwa na mada isemayo: “Mafanikio ya Kielimu na Maarifa ya Hawza ya Kidini ya Najaf Ashraf kuanzia Karne ya Tisa hadi ya Kumi na Mbili Hijria.” Liliandaliwa kwa msaada wa Sekretarieti Kuu ya Atabatu Abbasiyya Tukufu, kupitia juhudi za Kamati Kuu ya Kufufua Urithi wa Kielimu na Kituo cha Tafiti na Utafiti cha Sheikh Tusi, kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kielimu na Kifikra ya Al-Ameed, Chuo Kikuu cha Al-Kafeel, Chuo Kikuu cha Kufa na Chuo cha Imam Kadhim (as), tawi la Najaf.

Katika mkusanyiko huo wa kielimu, walishiriki kundi la wanazuoni na wataalamu kutoka Hawza za Qum na Najaf, wahadhiri wa vyuo vikuu na watafiti kutoka Iraq, Iran, Lebanon na vituo vingine vya kielimu. Washiriki hao walijadili nyanja mbalimbali za urithi wa kielimu na fikra wa Hawza ya Najaf katika kipindi cha karne nne zilizotajwa.

Sherehe za ufunguzi na uzinduzi wa vitabu vya kielimu na kitafiti

Sherehe za ufunguzi zilifanyika siku ya Alhamisi, tarehe 30 Mehr, katika ukumbi wa Sheikh Ansari, uliopo katika Jengo la Kifikra la Imam Murtadha (as), eneo la Hanana, mjini Najaf Ashraf. Katika hafla hiyo, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad al-Safi, msimamizi wa masuala ya kidini wa Atabatu Abbasiyya Tukufu, alitoa hotuba. Aidha, wawakilishi wa kamati za kielimu na maandalizi za kongamano hilo waliwasilisha hotuba zao.

Miongoni mwa vipengele muhimu vya sherehe za ufunguzi ilikuwa ni uzinduzi wa mkusanyiko wa vitabu na tafiti za kielimu vilivyochapishwa na Kamati Kuu ya Kufufua Urithi wa Kielimu, vinavyohusu urithi wa wanazuoni wa Hawza ya Najaf katika karne za tisa hadi kumi na mbili Hijria.

Vilevile, filamu maalumu ya makala iliyoonesha shughuli na hatua mbalimbali za maandalizi ya maadhimisho ya miaka 1,000 ya Hawza ya Kidini ya Najaf ilioneshwa kwa washiriki.

Kuwasilishwa makala 21 za kielimu katika nyanja mbalimbali

Katika vikao maalumu vya kielimu vilivyofanyika kwa siku mbili za kongamano hilo la maandalizi, yaliwasilishwa makala 21 za kielimu na kitafiti zilizohusu nyanja mbalimbali, zikiwemo Fiqhi na Usulul-Fiqhi, elimu ya Hadithi na Rijal, elimu ya Itikadi na elimu za kiakili, Qur’ani, lugha na fasihi ya Kiarabu, pamoja na historia ya urithi wa kielimu wa Hawza ya Najaf.

Katika sehemu iliyohusu elimu ya Hadithi na Rijal, ziliwasilishwa tafiti zilizokuwa na mada mbalimbali, zikiwemo:

- “Ubunifu wa kielimu wa Sahib Ma'alim katika elimu ya Rijal kupitia kitabu Muntaqa al-Juman.”
- “Sheikh Muhammad bin Ali Ardabili na kitabu Jami'u al-Ruwat.”
- “Misingi ya elimu ya Rijal kwa mtazamo wa Sheikh Abdullah Tustari.”
- “Majina yanayofanana katika elimu ya Rijal na njia za kuyatofautisha kwa mtazamo wa Sahib Madarik.”
- “Maswahaba wa Ijmaa kwa mtazamo wa wanazuoni wa zama za baadaye, hususan katika mwenendo wa kielimu wa Muhaqqiq Ardabili.”

Katika eneo la Fiqhi na Usulul-Fiqhi, ziliwasilishwa tafiti zilizohusu mada zifuatazo:

- “Nafasi ya kuiga mwenendo wa Maimamu Maasumina (as) katika kutoa hukumu za Fiqhi kwa mtazamo wa Sahib Madarik.”

- “Swala za Sunna katika wakati wa Swala za faradhi na Swala za kulipa kwa mujibu wa msingi wa kielimu wa Sahib Madarik.”

- “Mgongano wa wajibu wenye muda mpana na wajibu wenye muda maalumu, pamoja na athari zake katika kusihi kwa ibada kwa mtazamo wa Muhaqqiq Karaki, Muhaqqiq Naini na Ayatullah Khu'i.”

- “Mtazamo wa Muhaqqiq Karaki kuhusu mamlaka ya baba katika kufungisha ndoa ya binti aliyebalehe na mwenye utambuzi na uwezo wa kufanya maamuzi.”

Uchunguzi wa mbinu ya Fiqhi ya Faidhullah Tafreshi katika kitabu Al-Nur al-Qamariyya, pamoja na mafanikio ya kielimu ya Fiqhi ya Mirza Muhammad bin Ali Astarabadi, hususan katika kitabu Ayat al-Ahkam, pia vilikuwa miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika eneo hili.

Katika sehemu ya elimu ya Itikadi na elimu za kiakili, watafiti walijadili mada zifuatazo:

- “Mbinu ya kielimu ya Sheikh Khudhr Razi Hablurudi katika kitabu Miftah al-Ghurar.”

- “Mbinu ya kielimu na kiuhakiki ya Muhaqqiq Shirwani katika maelezo yake kuhusu masuala ya Itikadi na Falsafa.”

- “Umoja na tofauti ndani ya Umma wa Kiislamu kwa kuzingatia kitabu Dhiyau al-Alamin cha Allamah Futuni.”

- “Aya ya Wilaya na maana zake kwa mtazamo wa Allamah Futuni.”

Katika eneo la Qur’ani, lugha na fasihi ya Kiarabu, mada zilizochunguzwa zilijumuisha:

- “Mbinu ya tafsiri ya Fakhruddin Tureihi katika kuelewa Qur’ani Tukufu.”

- “Mbinu ya Sheikh Ahmad Jazairi katika kutoa hoja na dalili wakati wa kufasiri aya zinazohusu hukumu za kisheria.”

- “Mbinu ya Tureihi katika kuandaa majlisi za Imam Hussein (as) katika kitabu Al-Muntakhab.”

- “Diwani ya Sayyid Sadiq Fahham A'araji kama nyaraka ya kihistoria na kifasihi inayobainisha maisha ya kielimu na kijamii ya Najaf.”

Uzinduzi wa machapisho ya kielimu na kutambua mchango wa watafiti

Vikao vya siku ya pili vilifanyika katika Chuo Kikuu cha Al-Kafeel, ambapo watafiti waliwasilisha makala zao na kujadili mafanikio ya kielimu ya wanazuoni wa Hawza ya Najaf.

Katika sherehe za kufunga kongamano hilo, wawakilishi wa kamati za kielimu kutoka taasisi zilizoshiriki walitoa hotuba, mapendekezo ya mwisho ya kongamano yaliwasilishwa, na watafiti pamoja na wote waliochangia kufanikisha tukio hilo la kielimu walitambuliwa na kuheshimiwa.

Aidha, katika mwendelezo wa shughuli zinazohusiana na mkusanyiko huo, kundi la wanazuoni kutoka Hawza ya Kidini ya Qum walioshiriki katika kongamano la maandalizi lilifanya ziara tarehe 4 Aban 1405 Hijria Shamsia kwa Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Ahmad al-Safi.

Katika mkutano huo, walijadiliana kuhusu shughuli za kielimu na miradi ya Atabatu Abbasiyya Tukufu inayolenga kufufua na kuhifadhi urithi wa Hawza za Kidini. Vilevile, baadhi ya watafiti walimkabidhi Sayyid Ahmad al-Safi vitabu na machapisho yao ya kielimu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha